Friday, September 8, 2017

NANI ANAWEZA KUWA MLEMAVU?


Ulemavu hauchagui mtu, kabila, jinsi, dini wala cheo cha mtu. Jambo la muhimu kukumbuka ni kwamba mtu anaweza kupata ulemavu kabla ya kuzaliwa, wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa.
Jambo lingine muhimu la kukumbuka ni kwamba ukiwajali, kuwapenda na kuwa na ufahamu mzuri juu ya watu wenye ulemavu utakuwa umejiwekea akiba ya heshima ya utu wako, utu wa ndugu zako na utu wa watu wako wote wa karibu nawe. Siku itakapotokea wewe mwenyewe umepata ulemavu ujikubali na kujiona mtu.

Kumbuka; kumkataa mtu mwenye ulemavu kwa njia yoyote ile ni kujiimarishia misingi ya kujikataa wewe mwenyewe au kumkataa ndugu yako wa karibu atakapopata ulemavu. Jamii yako inapoongezeka kwa idadi ndipo na uwezekano wa kuwa na watu wenye ulemavu ni mkubwa.

Wakubali na wapende watu wenye ulemavu popote walipo!
Image may contain: 1 person, standing and sunglasses

Monday, September 4, 2017

Utata wa Dhana ya Ulemavu

Image may contain: one or more people and phone



Watu wengi duniani wameshindwa kuelewa dhana ya ulemavu. Wengi wao wameuchukulia ulemavu kuwa ni jambo la ajabu sana na kwamba watu wenye ulemavu pia ni wa ajabu. Hii sio sahihi.

Maana ya Ulemavu

Ulemavu ni hali ya kuwa na hitilafu ya kudumu mwilini au akilini inayomzuia mtu kutekeleza shughuli zilizo kawaida katika maisha ya jamii. Ulemavu unamwekea mtu mipaka asiweze kutekeleza shughuli fulani katika maisha yake, tofauti na watu wengine.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeunda mfumo wa kupanga alama (viashiria) za ulemavu. Hapa kuna tofauti kati ya

1. Hitilafu (kwa Kiingereza "impairment") kama kukosa uwezo wa kutumia kiungo cha mwili kama ilivyo kawaida.

2. Ulemavu (kwa Kiingereza "disability") kama hitilafu inayosababisha kukosa uwezo wa kutekeleza shughuli zinazotekelezwa na "watu wa kawaida".

3. Hasara au kikwazo (kwa Kiingereza "handicap") inayoweza kupatikana kwa mtu mwenye ulemavu akishindwa kutekeleza shughuli katika jamii.

Kwa mtu mwenye ulemavu kuna mambo matatu; Hitilafu, Ulemavu na, Vikwazo katika utendaji wa kila siku. Hapa ndipo wazo kupata vifaa saidizi lilianzia.


Sunday, September 3, 2017

HUISHA


Zawadi pekee kwa binadamu ni uhai tulio nao!

Uhai ndio unatuwezesha kuwa na utashi wa kufikiri tupendavyo, kutenda tuwezavyo na, kujijengea utamaduni tuupendao.

Binadmu amebarikiwa kwa uhai wake kuwa na maumbile mbalimbali, kuweza kutofautiana kwa urahisi kutoka binadamu mmoja hadi mwingine. Wapo watu wafupi, warefu, weusi, weupe, wenye ulemavu na wasio na ulemavu. Heshima ya mtu mmoja imetokana na uwepo wa mwenzake.

Leo tuishie kwa kusema: "Tuitumie vizuri zawadi ya uhai tulio nao."
Uhai wa mmoja usiwe taabu kwa maisha ya mwingine!

1. Tuhuishe utamaduni bora wa kufikiri
2. Tuhuishe heshima ya binadamu
3. Tuhuishe nia, ndoto, uwezo, ubunifu na kila aina ya nguvu (kiuchumi, kisiasa na kijamii) iliyo katika mtu mwenye ulemavu kwa maendeleo ya taifa na ya mtu mmoja mmoja.
4. Tuwape nafasi ya kutenda wanachokiweza.

Monday, January 30, 2017

Thamani ya Binadamu ni ipi?

1. Thamani ya binadamu imekaa Kiuungu zaidi

Mwanzo 1:26
"Mungu akasema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu..."

Kwa hiyo thamani ya ubinadamu imetoka kwa Muumba wake, yaani Mungu.

2. Maumbile ya Binadamu ni utashi wa Mungu mwenyewe

Kutoka 4:11
"...ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi BWANA?"

Kwa hiyo ulemavu ni sehemu ya Uumbaji wa Mungu.

3. Ulemavu si matokeo ya dhambi

Yohana 9:1-3
"...Huyu hakutenda dhambi, wala wazazi wake..."

Kwa hiyo tusimlaani (kumkataa) mwenye ulemavu kwa kuwa muumbaji wake amemkubali

4. Kumnyanyasa mwenye ulemavu ni chukizo kwa Mungu

Kumbukumbu La Torati 27:18
"Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia yake..."

Kwa hiyo kila afanyaye hila kwa mtu mwenye ulemavu kwa sababu ya ulemavu wa huyo mtu, huyo mtenda kosa atakataliwa na Mungu

5. Mungu huwa karibu na wenye ulemavu

Ayubu 29:15
"Nalikuwa macho kwa kipofu, Nalikuwa miguu kwa aliyechechemea."

Kwa hiyo pamoja na kwamba mtu anakuwa na ulemavu lakini Mungu ameweka uwezo wake kwake ili mtu huyo mwenye ulemavu aweze kufanya mambo makuu kwa uweza wa Mungu. Ndiyo maana unakuta mtu ni kipofu lakini amesoma hadi kufikia ngazi ya u profesa, mtu kiwete lakini anakuwa rais wa nchi (kama Frankline Delano Roosevelt-Rais wa zamani wa Marekani).

Hitimisho:
Mimi na wewe ni akina nani hata tuwakatae watu wenye ulemavu? Hata tukate viungo vyao? Hata tuwajengee daraja lao la ubinadamu?

Tumheshimu Mungu aliyetuumba wote, wenye ulemavu na wasio na ulemavu.

Ubarikiwe!

Saturday, December 31, 2016

Happy New Year with inclussive awareness


Words with no actions are over!
The World of unfulfilled promises is over!
Isolating contexts are wiped away!

What is being waited for is everything that makes possibilities for every inclusive vantage for people with disabilities! Let's all of us be the faithful agents, the part and parcel of creating a bright year 2017, indeed, to mold the year for all people in which the fruits are enjoyed  mutually!

Happy New Year To You All!

Stay Blessed!

Saturday, December 10, 2016

Kamata sana hii elimu

Katika elimu ambazo zinaogopwa ni hizi zinzohusu masuala ya ulemavu. Mtu anahisi akiifuatilia anaweza akaupata ulemavu. Hakika ulemavu unawapata watu, lakini si wote wanaweza kuathiriwa na ulemavu kwa kiwango kinachofanana. Ugumu unakuja kuwa "ni nani anayefuata kwa kupata ulemavu (kwa wasio na ulemavu)?"

Umuhimu wa elimu hii upo hapa:
1. Hii ni elimu ihusuyo afya ya mwili wako
2. Elimu hii inasaidia kuepuka mazingira hatarishi ya kupata ulemavu wa aina fulani fulani (mfano: ulemavu unaotokea kwa kutozingatia lishe bora).
3. Elimu hii juu ya ulemavu inasaidia kuwa na mtazamo chanya juu ya binadamu wengine wenye ulemavu.
4. Elimu hii ni sawa na huduma ya kuganga mioyo ya watu walioathiriwa na ulemavu kwa namna moja ama nyingine. Nimejifunza mambo mengi juu ya jamii ya watu wenye ulemavu na familia zao.

Ushuhuda wa kweli:
Kuna siku nikiwa natembea mtaani nilisimama kusalimiana na jamaa zangu. Mtu mmoja akasema "mtu yule mbona anaachwa kutambaa mtaani kwa shida"?. Huyu jamaa yangu alimaanisha kuwa ni kitendo cha aibu sana kwa mtu mwenye ulemavu kuonekana mtaani. Mimi nilianza kwa kusema: Hawa watu wanaokaa na huyu mtu wana akili sana, wana utu na wanampenda mtu wao. Nikamalizia kwa kusema: "Ulemavu ukiupokea vibaya unaweza ukawa masikini".
Katika kundi lile alikuwepo jamaa ambaye alishaathiriwa na ulemavu wa mwanae kwa miaka kadhaa. Akanishika mkono akanipeleka pembeni na kuanza kunihoji.

Miongoni mwa mambo aliyoniambia ni kuwa amehangaika na huyo mwanae kwa waganga hadi akafilisika, amekimbia kutoka Arusha na kwenda Morogoro kwa kuogopa aibu kwa marafiki zake. Akaongeza kusema kuwa mwanae huwa anamfungia ndani akienda kufanya shughuli zake. Nilipomwelekeza namna ya kuishi na huyo mwanae mwenye ulemavu alinielewa na kuishia kusema "mzigo nimeutua sasa".

Wapo watu wengi waliokosa huduma kama hizi, wanapata shida kwa kutokujua jinsi ya kuishi na jamii za watu wenye ulemavu na pia kupata shida ya kujifikiri juu ya ulemavu wao.
5. Ni elimu inayomhusu mtu mwenye ulemavu ajikubali jinsi alivyo, watu wanaotunza wenzao wenye ulemavu wasijisikie vibaya na kuwajengea utamaduni watu wasio na ulemavu jinsi ya kufikiri kivingine bila kuzingatia mapokeo mabaya juu ya watu wenye ulemavu. Ni kweli kila apataye ulemavu amelaaniwa? Amefanya kosa? Kwanini atengwe? Kwanini aonekane si binadamu? Ndiyo aonekane hawezi? (Haya ndiyo ya kujirekebisha).

Naendelea kukutia moyo wa kusoma maandiko haya kila upatapo nafasi ya kufanya hivyo.


Tengeneza Maana kwenye uwanja wa fujo






Utamaduni una nguvu kwenye maisha ya binadamu, naam, ndiyo maisha yenyewe! Tunaishi kutokana na utamaduni tuliojiwekea.

Jamii nyingi za Kitanzania hazipendi kufanya mijadala juu ya watu wenye ulemavu. Huu ni utamaduni wa jamii zetu katika ngazi za kaya, ukoo, kabila na hata kuakisi taifa zima.

Kutokana na utamaduni huu wa kutokufanya mijadala mingi juu ya ulemavu na watu wenye ulemavu kuwa ni mwiko (taboo) kuongelea masuala ya ulemavu. Kutoka hapa ndipo pamezaliwa, kukua na kukomaa kwa mizizi ya unyanyapaa kwa watu wenye mahitaji maalum.

Kama taifa, tunahitaji watu wenye roho ngumu za kutengeneza maana ya maisha kwa watu wenye mahitaji maalum na kwa watu wote ambao kwa namna hii au ile wameathiriwa na ulemavu (mfano: wazazi na walezi wenye watoto wenye ulemavu). Tunahitaji watu watakaotoa huduma ya kuwawezesha wahanga hawa kupumzika kisaikolojia (psychological comfort). Huduma hii ni adimu sana hapa nchini.

Kama kwenye vita za risasi na mabomu wapo watu wenye kujipatia ajira kwa vita hizo (mfano waandishi wa habari), je, si rahisi sana kupata ajira ya kutangaza habari za amani, mshikamano na upendo ndani ya nchi yetu wenyewe? Naam, inawezekana!

Wapo watu wengi wenye mahitaji maalum ambao wanatafuta neno la kuambiwa 'unaweza' na hawapati. Wapo wazazi na walezi ambao wanataabika kisaikolojia kwa kutokujua namna ya kukaa na watoto wao wenye mahitaji maalum- wanashindwa kupata mtu wa kusema 'mwanao ni mzuri na anaweza kufanya abcs'.

Sote tufikiri juu ya hilo!