Siku zote maisha ya mwanadamu kwa enzi zote yanategemea mawasiliano. Watu wanapata mitazamo mipya na mafanikio ya hali ya juu kijamii, kisiasa na kiuchumi kwa sababu ya mawasiliano.
Pia ikumbukwe kuwa mtaala (curriculum) wa nchi hutegemea mambo matatu muhimu ili uwe kamili, yaani; mahitaji ya wananchi wake (needs of people), mtazamo wa dunia (world view), na jumla ya maarifa yatolewayo (body of knowledge).
Nimejaribu kuangalia mfumo wetu wa mtaala wa elimu nikaona kipengele cha mahitaji ya binadamu hakijawekewa msisitizo kwa usawa wa binadamu wote. Chunguza, mathalan kwa wanafunzi viziwi (deaf students), wenye upofu (visually impaired students), na viziwi-vipofu (deaf-blind). Mawasiliano ya hawa wanafunzi yanategemea njia kuu za kitaalamu kama vile nukta nundu (kwa vipofu na viziwi-vipofu), na lugha ya alama (kwa viziwi na viziwi-vipofu).
Wenye uzoefu wa masuala ya elimu maalum watakuwa mashahidi ya kuwa, wanafunzi wenye aina ya ulemavu nilioutaja wana aina mbili tu za makundi ya watu wanaowasiliana nao kwa ufasaha; kundi la kwanza ni la walimu wao wenye taaluma ya elimu maalumu, na la pili ni la wanafunzi wenzao wenye ulemavu unaofanana.
Utafiti uliofanywa na Hakielimu, Disemba
2008 kuhusu Elimu Jumuishi na jinsi watoto wenye ulemavu wanavyoweza kufikia
malengo yao ya elimu unaonyesha kuwa ni 2% tu (asilimia mbili tu) ya walimu
wote waliohojiwa walisema ni wanaikubali elimu jumuishi kwa dhati (strong
agree). Sababu ya walimu wengi kukataa elimu jumuishi (takriban 98%) ilikuwa ni kukosa
utaalamu wa kuwasiliana na wanafunzi wenye ulemavu, hasa wasioona na vipofu.
Sote ni mashahidi kuwa mwanafunzi/mtu kipofu au kiziwi au kiziwi-kipofu awapo mazingira mengine ya kijamii tofauti na shuleni huwa ni tatizo kwa mawasiliano. Watu wengi ambao huwa nao kwenye mazingira mbalimbali hawajui lugha ya alama na nukta nundu. Hili ni tatizo, na huondoa haki ya mawasiliano kwa watu wenye aina hii ya ulemavu uliotajwa.
Hoja Yangu
Mtaala wa elimu nchini uweke mkakati wa kufundisha somo la elimu maalumu litakalowawezesha wanafunzi wote kufahamu aina mbalimbali za ulemavu zikiwamo za upofu na ukiziwi sambamba na namna ya mawasiliano yao (lugha ya alama na nukta nundu). Mfumo huu utazalisha kizazi chenye kujali mawasiliano kwa binadamu wote ili kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na pia kwa taifa zima la Tanzania.
Fikiri Kijumuishi ~~~ Tenda Kijumuishi ~~~ Jenga Taifa Jumuishi!
No comments:
Post a Comment