Lowassa awapa matumaini bodaboda
JESHI la Polisi, Kikosi cha
Usalama Barabarani, lipo katika mazungumzo na waendesha bodaboda ili kuangalia
namna ya kuimarisha usalama barabarani, na kupunguza vitendo vya ukiukwaji wa
haki za binadamu, vinavyofanywa na baadhi ya askari usalama barabarani kwa watu
hao.
Hayo yalielezwa jana,
wakati akizungumza kwenye tamasha la Siku ya Waendesha Bodaboda Dar es
Salaam (Bodaboda Day), lililofanyika katika viwanja vya Leaders na kudhaminiwa
na Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF) na Clouds Media Group.
Lowassa ambaye ni mbunge wa Monduli, alisema bodaboda ni ajira
kwa vijana wengi waliokuwa mitaani, na hivyo ni vyema ikawa na mfumo rasmi,
utakaowatambulisha na kuwasaidia kupata fursa mbalimbali za kiuchumi.
“Nimefanya mazungumzo na Mohamed Mpinga (Kamanda wa Kikosi cha
Usalama Barabarani), na kuangalia ni namna gani ya kuwasaidia vijana wa
bodaboda, amesema inawezekana, na sasa yupo katika mazungumzo na wadau wa
bodaboda ili kuboresha usafiri huo.
“Kuna baadhi ya askari wa usalama barabarani ni wavunjaji wa
sheria, wanaongoza kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu, lakini pia
vijana wa bodaboda lazima waheshimu kazi yao kwa kufuata sheria ili kuifanya
kazi hiyo iweze kuthaminika, na nawaahidi mkifuata sheria kama
tulivyokubaliana, kila mmoja atapata pikipiki yake,” alisisitiza.
Alisema tatizo la foleni kwa Mkoa wa Dar es Salaam ni
changamoto, na endapo bodaboda zikitumika vizuri, zitasaidia kupunguza adha
hiyo na kuinua uchumi wa nchi.
Lowassa alisema uchunguzi wa awali unaonyesha kwamba asilimia 50
ya waendesha bodaboda si wamiliki, hivyo wanaandaa harambee itakayosaidia
kuanzisha Saccos ili vijana wamiliki pikipiki zao binafsi.
Meneja wa Uchangiaji wa Hiyari PSPF, Mwanjaa Sembe, alisema
wameamua kuwasaidia waendesha bodaboda na kuwaelimisha juu ya utamaduni wa
kujiwekea akiba kwa maisha yao ya baadaye.
“Mafao yetu ni tofauti na mifuko mingine, na inawajali
wafanyakazi wa serikali, sekta binafsi na hata mtu mmoja mmoja, sio tu
bodaboda, lakini Watanzania wote wajifunze kuwa na utaratibu wa kujiwekea
akiba,” aliongeza Mwanjaa.
Mmoja wa waandaaji wa tamasha hilo, Dennis Lucas, alisema nia ni
kuunda umoja wenye manufaa, kwa kuelimishana na kutafutiana fursa, hususan
kwenye mikopo, ili kuinua uchumi wa vijana nchini.
No comments:
Post a Comment